Wednesday, April 23, 2014

UKAWA WAKANUSHA MADAI YA BAADHI YAO KURUDI BUNGENI NA KUDAI POSHO

UKAWA: HAKUNA UKAWA ALIYERUDI BUNGENI WALA ALIYEENDA KUOMBA POSHO

Julius Mtatiro

Nimesikitishwa sana na kauli iliyotolewa bungeni leo kwamba UKAWA wamerejea bungeni na wamefikia kudai posho.
Naomba watanzania watambue kuwa kauli hiyo ni mwendelezo wa propaganda za CCM dhidi ya wale wanaotetea na kutaka baadhi ya maoni ya msingi yaliyomo katika rasimu ya katiba yaheshimiwe na kuboreshwa.
Tangu tumeondoka bungeni tumekuwa tukiendelea na vikao maalum vya kistratejia Zanzibar na katika mikoa 10 ya Tz bara. Baada ya vikao hivyo tutawatangazia wananchi ratiba ya shughuli zetu.
UKAWA inaundwa na wajumbe zaidi ya 200, lakini baada ya kutoka bungeni kuna wale ambao walikubali kuondoka lakini walipofuatwa na waziri mkuu na mawaziri usiku huohuo wakabadilisha mawazo na kuamua kubaki.
Hawa wamo kina Isack Cheyo na wengine wanaotoka katika vyama visivyo na wabunge. Sisi tunaheshimu maamuzi yao.
Asilimia 95 ya wajumbe wote wa UKAWA hawajarejea bungeni na wako maeneo maalum wakiendelea na vikao vya maandalizi. Baadaye tutakutana sote na kuanza kazi ya kuwaendea wananchi kidemokrasia.
Ikiwa kuna mjumbe wa UKAWA ameenda kuomba apewe posho tunamuomba mwenyekiti wa bunge maalum amtaje kwa majina vinginevyo atakuwa anadanganya. Huwezi tu kusema ati UKAWA wamerudi kuomba posho, au wamerejea bungeni, wataje waliorejea.
Msimamo wa UKAWA unajulikana, hatutaki kuwa sehemu ya watu wanaidharau maoni ya wananchi na waliokutana kwa ajili ya matusi na kila aina ya ubaguzi. Pia tumekataa kuwa sehemu ya watu walioacha kujadili nyaraka walizoletewa na matokeo yake wanajadili waraka wao walioletewa na CCM.
Kuna watu wanadhania hili tunalolifanta leo lazima liwe na majibu leo, la hasha! Hili linaweza kuwa na umuhimu kesho, watu wengi huangalia leo na husahau kesho, sisi tumeamua kuangalia kesho na keshokutwa na wanaotubeza watapongeza tulichokifanya sasa siku zijazo.
J. Mtatiro,
Katibu wa UKAWA.

No comments:

Post a Comment